Utajiri Uliojificha – Zao la Embe Ndio Habari Mpya Katika Sekta ya Kilimo!

  • Home
  • News
  • Utajiri Uliojificha – Zao la Embe Ndio Habari Mpya Katika Sekta ya Kilimo!

Mkuranga, Tanzania – Katika eneo la Mkuranga, shamba moja la maembe limekuwa kivutio cha kuvutia kwa wakulima, watafiti, na vijana wanaotaka kujifunza kilimo cha kisasa.

Shamba la Maembe: Mfano wa Kilimo cha Kisasa
Shamba hili, lenye maembe ya aina mbalimbali, limekuwa kituo cha mafunzo kwa vijana na wakulima wanaotaka kujifunza mbinu za kisasa za kilimo. Geoffrey Kirenga, Mkurugenzi Mtendaji wa SAGCOT, alisema kuwa shamba hili ni mfano wa jinsi kilimo cha kisasa kinaweza kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya kilimo nchini.

“Hili ni shamba la maembe ambalo linaonyesha uwezo wa kilimo cha kisasa. Tunataka vijana na wakulima waje hapa kujifunza namna ya kufanya kilimo cha maembe kwa ufanisi na kwa faida,” alisema Kirenga.

Aina za Maembe Zinazostawi Tanzania
Hamadi Mkopi, mtaalamu wa kilimo cha maembe, na mumiliki wa shamba hili, alitoa maelezo kuhusu aina tatu za maembe zinazostawi katika shamba hilo:

  1. Keitt: Hii ni aina ya embe inayopendwa sana duniani kwa uzazi wake mzuri na uwezo wake wa kukaa kwenye soko kwa muda mrefu. “Keitt ni embe ambalo linaweza kuzalisha hadi tani 70 kwa hekta moja. Linastawi vizuri Tanzania na lina soko kubwa kimataifa,” alisema Mkopi.
  2. Chokanan: Asili ya Malaysia, embe hili lina rangi na umbo la kuvutia, na linastawi vizuri Tanzania. “Chokanan ni embe lenye soko zuri hasa kwa sababu ya umbo lake la kipekee na ladha yake nzuri,” aliongeza Mkopi.
  3. Sindhri: Asili ya Pakistan, embe hili ni maarufu kwa ubora wake na soko lake kubwa Ulaya na Mashariki ya Kati. “Sindhri ni embe bora sana na tunalipanda hapa kwa majaribio. Linastawi vizuri na lina uwezo mkubwa wa kuingia kwenye soko la kimataifa,” alisema Mkopi.

Hatua za Kukuza Miche ya Maembe
Shamba hili pia linazalisha miche ya maembe kwa ajili ya wakulima. Mkopi alieleza hatua mbalimbali za kukuza miche hiyo, kuanzia kuchagua mbegu bora, kupanda, na kufanya grafting ili kuhakikisha kuwa miche inayotolewa ni bora na inayostawi vizuri.

“Tunafanya uchambuzi wa mbegu na kugredi kwa ukubwa na umri. Tunatarajia kufanya grafting kwenye mwezi Machi na kuanza kusambaza miche kwa wakulima,” alisema Mkopi.

Fursa kwa Vijana na Wakulima
Kwa mujibu wa Kirenga, kilimo cha maembe kina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko kijamii na kiuchumi. “Vijana wanaweza kujiunga na sekta hii na kujenga maisha bora. Maembe yana soko kubwa ndani na nje ya nchi, na hii ni fursa kubwa kwa wakulima wa Tanzania,” alisema Kirenga.

Shamba hili la maembe limekuwa kielelezo cha jinsi kilimo cha kisasa kinaweza kuleta mafanikio makubwa. Kwa kutumia mbinu za kisasa na kuchagua aina bora za maembe, wakulima wa Tanzania wanaweza kufanikisha biashara zao na kushiriki katika soko la kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *