Raha Farm Yafungua Kituo Kipya Kahama, Ikikuza Sekta ya Nyanya Tanzania

  • Home
  • News
  • Raha Farm Yafungua Kituo Kipya Kahama, Ikikuza Sekta ya Nyanya Tanzania

Kahama, Tanzania – Januari 29, 2025

Kampuni ya Raha Farm, inayojulikana kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya kilimo cha mboga mboga Tanzania, imefungua kitalu chake cha nne katika Manispaa ya Kahama, mkoa wa Shinyanga. Upanuzi huu, unaoongozwa na KIJANA MJASIRIAMALI na Mkurugenzi Mtendaji, Raha Aloyce, unadhihirisha dhamira ya kampuni hilo katika kuwawezesha wakulima, kuendeleza kilimo endelevu, na kusaidia Tanzania kujijenga kama mshindani mkubwa katika soko la nyanya duniani.

Uzinduzi wa kitalu hicho uliofanyika katika eneo la Nyakato, ulifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mheshimiwa Mboni Mhita na kuhudhuriwa na mamia ya wadau wakiongozwa na Mbunge wa Jimbo la Kahama Mhe. Jumanne Kibera Kishimba. Wengi wa wadau walitokea sekta mbalimbali ikiwa ni pamoja na wakulima kutoka Kanda ya Ziwa, maafisa wa serikali, wasambazaji wa pembejeo za kilimo, na vikundi vya wakulima. Hafla hiyo ilisisitiza ushirikiano thabiti kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kusukuma mbele kilimo endelevu nchini.

Kuongeza Uzalishaji Kupitia Miche Bora

Utafiti mbalimbali katika Afrika Mashariki umeonyesha kuwa matumizi ya miche bora na yenye ustahimilivu kwa magonjwa huongeza uzalishaji wa nyanya kwa kiwango kikubwa. Kwa mfano, katika mkoa wa Morogoro, wakulima waliotumia miche iliyoboreshwa waliripoti kuongezeka kwa mavuno kutoka wastani wa tani 10 kwa hekta hadi tani 25-30 kwa hekta, sawa na ongezeko la 150-200% (kwa mujibu wa IITA na TARI).

Nchini Kenya, kuanzishwa kwa aina mpya za mbegu za nyanya katika ukanda wa Rift Valley kumeongeza uzalishaji kutoka tani 15 kwa hekta hadi tani 40 kwa hekta, ongezeko la 167% (IITA, Shirika la Utafiti wa Kilimo na Ufugaji Kenya [KALRO]). Katika Ethiopia, wakulima katika mkoa wa Oromia wameongeza mavuno kutoka tani 10-12 kwa hekta hadi tani 35 kwa hekta, ongezeko la 200-250% (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Ethiopia [EIAR], FAO).

Mchango wa Mkakati Huu kwa Sekta ya Nyanya Tanzania

Kampuni ya Raha Farm inaendesha mkakati wa kukuza mbinu bora za kilimo, likiwa mshirika wa mpango wa SAGCOT (Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania). Dhamira yake ya kuwawezesha vijana na kuongeza tija inang’ara katika uzalishaji kupitia mbinu zake za usimamizi wa vitalu, utayarishaji wa miche, na mbinu bora za upandaji. Hivyo basi, upanuzi wake hadi Kahama unaleta rasilimali muhimu na utaalamu kwa wakulima wa Kanda ya Ziwa, husaidia kuongeza uzalishaji wa nyanya, kupunguza hasara baada ya mavuno, na kujenga soko lenye ushindani zaidi kwa wakulima wa Tanzania.

Mheshimiwa Mboni Mhita, Mkuu wa Wilaya (aliyevaa miwani) akiwa kwenye Kitalu-nyumba kipya cha Kampuni ya Raha Vegetable Farm katika Manispaa ya Kahama, akishuhudia mbinu muhimu za kilimo kutoka kwaRaha Aloyce, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo wakati wa uzinduzi wa Kitalu hicho tarehe 29 Januari, 2025. Upanuzi wa Kampuni hiyo unalenga kuwawezesha wakulima na kuendeleza ukuaji wa kilimo endelevu katika eneo hilo, huku ikitanabaisha uzoefu wake katika kilimo endelevu na mchango wake katika sekta ya kilimo cha mboga nchini Tanzania..

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *