SAGCOT na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Zawajengea Wakulima Uwezo Kupitia Ziara ya Mafunzo katika Mashamba ya Mfano ya Njombe

  • Home
  • News
  • SAGCOT na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Zawajengea Wakulima Uwezo Kupitia Ziara ya Mafunzo katika Mashamba ya Mfano ya Njombe

Gairo, Morogoro

Mnamo mwezi Aprili 2024, SAGCOT, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, iliwezesha ziara ya mafunzo kwa wakulima wapatao 40 na maafisa ugani 4 kutoka halmashauri za wilaya za Gairo na Morogoro. Ziara hiyo iliwapeleka wakulima kutembelea mashamba ya mfano ya wakulima waliyonufaika na SAGCOT katika Mkoa wa Njombe.

Wakati wa ziara hiyo, wakulima wa Morogoro walipata fursa ya kuona jinsi mashamba ya parachichi na viazi mviringo yanavyotunzwa kitaalamu hadi kufanikisha mavuno ya tani 40 za viazi kwa eka na tani 20 za parachichi kwa eka.

Wakulima wenyeji kutoka Njombe walielezea kwa vitendo jinsi ya kuandaa vitalu vya parachichi na kutunza miche bustanini hadi inapohamishiwa shambani. Aidha, kwa mazao ya viazi, walijifunza mbinu za uandaaji wa mbegu, kutoka kwa wasambazaji wa mbegu za kisasa, namna bora ya kuandaa mashamba, na utunzaji wa mazao shambani hadi mavuno kwa kutumia zana za kisasa.

Baada ya kurejea kutoka kwenye mafunzo hayo, SAGCOT iliwaleta wakulima walimu kutoka Njombe ili kuwafundisha wakulima waliokuwa kwenye ziara wakiwa katika mashamba yao Gairo na Morogoro kwa muda wa wiki moja. Fursa hii iliwezesha wakulima wote kutambua mbinu bora za kilimo, ikiwa ni pamoja na:

  • ✅ Kupima afya ya udongo
  • ✅ Kuandaa vitalu vya miche
  • ✅ Kupanda na kutunza miche ya parachichi

Hadi kufikia Desemba 2024, jumla ya miche 400,000 ya parachichi ilikuwa imepandwa na wakulima wa mfano wilayani Gairo. Pia, ekari 58 zilikuwa zimepandwa parachichi katika kata za Masenge na Lukinga.

Vilevile, katika Wilaya ya Gairo, ekari 10 za mashamba darasa ya viazi mviringo zimeanzishwa chini ya usimamizi wa karibu wa Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Mhe. Jabiri Makame. Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Mhe. Adam Kighoma Malima, amejiunga rasmi na vikundi vya wakulima wa viazi na parachichi katika wilaya hiyo.

Kauli za Viongozi wa Wakulima

Akizungumza na Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia Viwanda, Biashara, Mazingira na Kilimo, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Deo Mwanyika, Mbunge na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, mnamo 15 Februari 2025, Mwenyekiti wa Kikundi cha Muungano kutoka Kata ya Lukinga, Bwana Phillipo Lukonga, alisema:

“Nafurahi kuona kwamba Mhe. Mkuu wa Mkoa wetu amekuwa mwanachama wetu katika kikundi. Sasa tunatunza mashamba kitaalamu. Tulihamasika kufanya kilimo cha kisasa cha parachichi baada ya kupata fursa ya mafunzo kutoka kwa SAGCOT, ambayo ilitupeleka ziara ya mafunzo Mkoani Njombe. Kwa sasa, tunayo miche 5,800 ambayo tayari imetoa maua katika mashamba ya wanachama wetu, na tunasubiri kupandisha vikonyo kwenye miche mingine 1,200 ili tuendelee kupanua mashamba yetu.”

Hitimisho

Kamati ya Bunge ilijionea ari kubwa ya wakulima wadogo ambao wako tayari kuwekeza katika mazao mapya ambayo awali hayakuwa yakilimwa katika maeneo yao. Wakulima hawa wana imani kuwa Serikali na wadau wengine wataendelea kuwaletea fursa za maendeleo.

Kwa upande wake, SAGCOT itaendelea kusaidia mapinduzi ya kilimo kwa kuhamasisha fikra mpya, kuibua mazao mapya yenye tija, na kuhakikisha kilimo kinakuwa endelevu kwa wakulima na mazingira husika.

SAGCOT – Transitioning into Agricultural Growth Corridors of Tanzania – AGCOT

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *